juu

Wednesday, 31 July 2019

kelele za mbu hazinyimi usingizi

WALETEEEE KELELE shogaa wanakwambia chakula cha harusini hakishibishi na ukitaka kujua masikini na tajiri ufike muda wa zawadi kwa maharusi, wareeee reeee! Miye tena niliokosa zipu kwenye mdomo, linalopita mbele yangu naongea tu kwani uongo jamani! Heri yetu tukiamka midomo inanukia wewe je, ukiamka tunaanza kutafutana kama siyo kuulizana shimo la jalala limefukuliwa upya? Au gari la taka limeangusha uchafu!  Ona sasa hadi nimesahau kukusalimia, mzima msomaji wangu wa kona hii ya Shangingi Mstaafu Anti Naa? Kwa uwezo wa manani nina imani wote hamjambo wazima wa afya kama kuna wagonjwa basi tuwaombee na kama kuna aliyetangulia mbele ya haki vilevile, tumuombee apokelewe kwa amani pia apate huruma ya Muumba.

Jama-ni leo nataka kuzung-umza na watu wazima wenzangu. Kwa vile ni watu wazima tutazungumza kwa lugha ya kiutu uzima lakini vikinipanda mtaniwia radhi kwa vile siwezi kuuzuia mzuka kama chafya ikija lazima niiachie mwenzangu! Naanza kuongea na wewe unayemnyima raha mwenzako kutokana na vitimbi unavyomfanyia.

Tena usinitumbulie macho kama wasindikizaji wa bibi harusi waliokosa sare za madera! Nachukia sana kama siyo kukereka! Jamani huu siyo wakati wa kuwapa nafasi wanawake waliokosa heshima na kujua nini thamani ya ndoa.

Wewe kama hujaolewa hebu heshimu ndoa za wenzako. Hata kama makosa kafanya mumewe kutoka nje ya ndoa, yeye ana kosa gani? Nyie wanawake mnaoingilia uhusiano wa watu, jaribuni kuziheshimu ndoa za wenzenu, si busara kumtukana mke wa mtu, kama ungekuwa bora ungeolewa wewe basi, upo?

Wengi wenu huwa hampendi ndoa, mnatanguliza starehe mbele na kufanya ugeuzwe chombo cha starehe na si mwanamke wa kuolewa. Hebu nikuume sikio muolewaji, kelele za mkosaji wala haziumizi masikio, shosti ni kosa kubwa kujibizana au kutukanana na mtu aliye nje ya ndoa yako, hiyo ni kumpa kichwa na kuamini ameweza kukuchokonoa na likakugusa.

Nikuibieni siri, wote walio ndani ya ndoa, kupatwa na masaibu ya kusumbuliwa na mahawara za waume zao. Hizo ni kelele za mkosaji, kupenda kwake starehe leo kumemfanya awe jamvi la mtaa, kapata raha kidogo kwa mumeo kachanganyikiwa sasa anataka kuingia ndani kabisa.

Hebu zichukulieni kelele zao kama mbu walio nje ya chandarua, wasio na uwezo wa kuwauma zaidi ya kupiga kelele, siku zote kelele za mbu hazikunyimi usingizi. Ushauri wangu kwenu kila anapotokea mtu wa kukutukana kwa vile tu wewe umeolewa na yeye kuachwa solemba hiyo si juu yako bali ya mumeo.

Kujiepusha na mtu huyu kwa kukaa kimya usimjibu kwa vile wewe umeishapata, ukimya wako ni pigo zito kwake kuliko kutukanana naye. Muache abwabwaje mwisho wake atachoka kama mbu nje ya chandarua, atakufa kwa kihoro, ukiona linakukera litue kisha lihifadhi! Haloo eeeh!

Mwisho nazungumza na ninyi wanaume msiojua thamani ya mwanamke ndani ya ndoa. Ni kosa kubwa kumlinganisha mkeo na hawara, kufanya hivyo ni kumdhalilisha mkeo. Mkomeshe hawara yako amheshimu mkeo kwani kama angekuwa yeye ni bora ungemuweka ndani.

Mwanaume mwenye tabia hizo ni zaidi ya mnyama, hufai kuwa baba wa familia. Kama ulikuwa bado una tamaa zako za mwili kwa nini ulikimbilia kuoa? Mjengee heshima mkeo ambaye ana dhamana kubwa mbele ya Mungu. Na wewe uliye nje ya ndoa heshimu ndoa ya mwenzako, kuiba penzi si kibali cha kuingilia ndoa ya mtu, uwe mtu wa aibu kama mbwa koko aliyekatwa mkia. Kwa leo niishie hapa, ni mimi Anti Nasra, Shangingi Mstaafu.

The post kelele za mbu hazinyimi usingizi appeared first on Global Publishers.




source https://sirinzitozamapenzi.blogspot.com/2019/07/kelele-za-mbu-hazinyimi-usingizi.html
Share:

0 comments:

Post a Comment

Translate

sam magelle

Main Menu Links

HABARI KALI ZAIDI

CHAGUA HABARI na sammagelle.com

Copyright © juu | Powered by Blogger