Upendo wa kweli,nguzo muhimu ya kuwa pamoja ni upendo.Kama miongoni mwenu(wenza au wanandoa) kuna upendo wa kweli ni rahisi sana kuweza kusawazisha mambo yanayowakabiri au vikwazo mnavyopitia kila siku.Kukubaliana na hali mbalimbali katika maisha kama vile shida na raha yote hiyo hutokana na upendo wa dhati baina yenu.Inaeleweka kuwa ni vigumu sana kwa wanandoa au wapenzi kutambua upendo au mapenzi ya kweli,lakini hiyo siyo shida sana maana njia rahisi ni kupitia matendo au maongezi anayo toa mwenza wako unaweza ukatathimini na kujua nini anamaanisha.
Ushirikiano(nafasi ya kujieleza),hii inahusu zaidi wakati wa kutoa maamuzi au uchangiaji wa mawazo katika kujenga wazo fulani.Kweli kuna wakati hutokea mmoja baina yenu humhitaji kutoa wazo lisilojadiliwa(ni kama kusema anataka kufanya kitu ambacho ni lazima kifanyike kama kilivyo bila nyongeza au punguzo lolote lile),lakini siyo kila muda inatokea hivyo au mara nyingi itokee hivyo.Kutokupata nafasi ya kujadiliana au kuchangia inaweza kutafsiriwa kuwa wewe huwezi chochote au mawazo yako hayana maana yoyote kwake, na ndipo uhusiano unapoanza kutetereka zaidi.
Umoja/mshikamano,kusimama pamoja wakati wote iwe wakati wa furaha au shida inaleta uhamasisho wa kuamini nia ya mwenza wako.Ni muhimu kusaidiana wakati wote wa maisha ingawa mnajuana namna mnaendesha maisha yenu,kosa kubwa ambalo wengi tunalifanya ni kufanya maisha ya kimazoea kwa mwenza wako kwa vile labda mnaishi pamoja(kwa wanandoa) na kuona hakuna umuhimu wa kumfariji au kumshauri.Ndio maana inapotokea mmoja wenu akachepuka(kutoka nje ya ndoa) atamwona mchepuko anamthamini sana kuliko aliyenaye ndani siku zote.
Imani na kuaminiana,ni muhimu na vyema kujenga imani ya kuwa mwenza wako anakupenda na anakuthamini kabla ya kuanza kukusanya mabaya yake tu.si kazi rahisi kuja kukubaliana na hoja hii,lakini cha muhimu ni kama ukishajua mwenendo wake wa kawaida unaweza kutatua matatizo yote yanayo kukabili kisaikolojiaau kifikra.Kumwamini mwenza wako ni njia pia ya wewe kuwa na msimamo makini pale unapokutana na vishawishi toka upande fulani ikiwemo kwa maisha ya kawaida, marafiki, wazazi au kimapenzi.Mara nyingi kutokuaminiana matokeo yake huwa ni kutoka nje ya ndoa au uhusiano kwa madai ya kukomoana na mwenza wako.Hilo huwa siyo suluhisho bali ni kuongeza tatizo jipya lisilo na majibu hasa pale itakapothibitika kuwa huyo mwenza wako hakuwahi kufanya hivyo.
Kipato,suala la kipato katika uhusiano au ndoa ni jambo lenye kipaumbele kikubwa na inaweza ikavuruga au ikajenga ndoa bora sana.Kwanza kipato hupunguza kuangukia katika vishawishi hasa kimapenzi(mapedeshee na mashuga mami<sugar mumy>).Pili huondoa migogoro ya wapenzi kama vile kugombea mahitaji muhimu(chakula, mavazi, malazi, afya).Tunaposema kipato haijalishi ni cha mtu mmoja au kwa ushirika wenu wote wawili,ili mradi inaweza kukidhi mahitaji yenu.
Uwazi na ukweli,kusema ukweli mbele ya mwenza wako kunadumisha sana uhusiano wenu na kuaminiana zaidi.Maana kama leo umedanganya na ukagundulika basi hata kesho ukisema chochote italazimu mwenza wako afanye upelelezi wa hilo jambo kwanza ndio akupe jibu.Kitu ambacho hata wewe mwenyewe kitakupa karaha na kuona unaonewa au hupendwi.
Uvumilivu na utulivu,katika uhusiano kuna milima na mabonde ya vikwazo mbalimbali.Kustahimili vikwazo ni lazima wewe mwenyewe kwanza uwe tayari kutokuwa mropokaji wa mambo hasa kwa mwenza wako.Ukipokea jambo lo.lote linalohusu mwenza wako ni vema ukatulia na kulichambua ukweli wake kabla ya kumparamia kwa ugomvi wakati hujui aliyekupa taarifa hiyo alilenga nini.Wapo watu ambao hutamani sana mgawanyiko wenu na siyo umoja mlionao,kwa hiyo ni muhimu kuchunguza sana mambo na siyo kukurupuka mana unaweza ukakosa hata ukweli wa jambo la kweli na ukaonekana ni mkorofi tu.
Kusamehe,upendo wa kweli hubebwa na kitu kinachoitwa msamaha.kukosekana kwa msamaha katika uhusiano ni wazi penzi lenu litaishia SHUBIRI.Hakuna binadamu mkamilifu,hivyo ni ukweli kuna wakati kosa litatokea lakini kama inawezekana jaribu kusamehe maana hata mwenza wako kuna mambo ambayo huwa anasamehe pengine hata kabla ya kukuuliza.Kumbuka kuwa kinara wa kupaisha mambo kwa mwenza wako inaweza ikamfanya naye aone kuwa ndio utaratibu au njia bora ya kufanya na siku ukikosa kidogo tu utaona namna anavyokuja juu hata utajiona labda hupendwi.
Kutunza na kupambanua mambo,unapopokea jambo lolote ni muhimu kulipambanua wewe binafsi na uchukue hatua za kufanya.Kupambanua ni kujiridhisha ukweli wa kitu husika na kupata suluhisho lake.Ni hatari kutunza matukio mengi akilini mwako bila ya kuyatolea utatuzi wake maana hupelekea kuleta hasira za haraka sana wakati unapopokea tukio jipya, hii inaweza kuleta mtafaruku wa haraka sana dhidi yenu.
Pia ni muhimu sana kujitambua na kutambuana baina yenu wenza au wapenzi,maana tumetoka familia mbili tofauti na kufanana kwenu mara nyingi ni kwa vitu muhimu tu kwa jamii.Kuna watu asili yao ni wasiri na wengine ni wepesi wa kujitangaza hasa kiuchumi au mipango,unapo kutana na mpenzi ambaye ni msiri ni vizuri ukaendana naye mtindo huo mana kutoa mambo yake hadharani kutakuletea migogoro muda mwingi na hata inaweza kuleta uvunjikaji wa uhusiano.
0 comments:
Post a Comment