juu

Friday, 6 September 2019

DALILI ZITAKAZOKUONYESHA UPO KWENYE MAHUSIANO MAZURI


Haijalishi ni kwa namna gani uhusiano umeanza au umeisha, kila mara tunapokuwa katika uhusiano lazima kuna somo tunajifunza.

Hakuna uhusiano ambao ni mkamilifu, lazima mtazozana kwa maneno au vitendo na wakati mwingine kugombana kabisa. Lakini kuzozana huko hakumaanishi kwa uhusiano wenu umefikia mwisho, japokuwa mkiwa watu wa kugombana kila siku, inabidi mkae chini mzungumze kuweza kufahamu tatizo ni nini.

Kuwa na furaha ni jambo moja, lakini kujua kuwa upo katika uhusiano ambao utadumu licha ya kuwa mnapitia magumu kiasi gani, ni jambo jingine ambalo kila mmoja analitamani.

Hapa chini ni ishara ambazo zinazungumza kuhusu uimara wa uhusiano wenu.

Mawasiliano
Kikubwa ni kujiuliza mnazungumza kuhusu nini na mna mazungumzo ya aina gani. Mnaweza mkawa mnazungumza kuhusu jinsi ya kufanya maamuzi, tabia nzuri ama mbaya zinazowakera au kuhusu maisha yenu ya mbeleni.

Chagua muda sahihi na mahala sahihi pakuzungumzia jambo lako, dunia haitaisha kama ukiamua kusubiri saa moja ili uweze kupata sehemu sahihi ya kuzungumza na mwenza wako. Fahamu unataka kusema nini, utakavyokisema na mazingira utakayosemea ili kuwa na mawasiliano madhubuti.

Makubaliano
Hii sio kwenye uhusiano wa kimapenzi pekee, hata kwa rafiki wa kawaida ni muhimu kuzingatia hili kwani huwezi ukawa kila mara wewe unapokea tu, lazima pawepo wakati wa wewe kutoa pia.

Mnapoingia katika uhusiano, kila mmoja huwa na tabia zake na uelewa wake juu ya mambo, lakini wapenzi ambao ni imara, watakaa na kujadili kuona namna bora ya kuweza kuchanganya tabia zao na kutoka na moja ambayo wote wataikubali.

Ukiwa wewe hutaki kubadilika ila unataka mwenzako ndio kila mara abadilike kufuata mawazo yako, hakika kila mara mtaishia kugombana.

Uaminifu na kusamehe
Vitu hivi viwili ni muhimu sana katika uhusiano wako, kila mmoja anatakiwa kuweka nguvu sawa kuhakikisha vinaendelea kuwa nguzo muhimu kati yenu wawili. Usiwe na nafasi ya kuwa na mawazo hasi na mwenzako, na unapokuwa na wasiwasi, mwambie na yeye akueleza ukweli pasi na kupepesa macho.

Jifunze kusamehe na kusahau, haiwezekani kwenye uhusiano kila mara nyie mkawa ni watu wa kugombana tu, mtapata wapi muda wa kufurahia uwepo wa mwenzio? Samehe na sahau vitu ambavyo hamuwezi mkaendelea kuvijadili. Haiwezekani mkawa mnaendelea kujadili tatizo lililotokea mwezi uliopita.

Jitambue
Hili huwakumba zaidi wanawake. Wanapoanza kuwa kwenye uhusiano, wapenzi wao huwa ndio dunia yao. Huwapoteza marafiki zao na kuacha kufanya vile vitu alivyokuwa akivipenda, na badala yake sasa anafanya vitu ambavyo mpenzi wake anavipenda.

Hii huwa haitokei sana kwa wanaume, ni mara chache sana utakuta mwanaume ameacha kuangalia mpira kwa sababu tu mpenzi wake hapendi aangalie.

Hakikisha unaendelea kuwa na marafiki, na kufanya vitu ulivyokuwa ukivipenda hata baada ya kuwa kwenye uhusiano. Hivyo vitakusaidia wewe endapo chochote kitatokea katika uhusiano wenu. Hata ikitokea mkaachana na huyo mpenzi wako, bado una marafiki wa kukusaidia.
Anakufanya ujisikie vizuri na mwenye furaha
Sio lazima uwe umejiremba ndio mpenzi wako aonyeshe kuvutiwa na wewe, hata kama ndio umeamka kutoka usingizi au umetoka kuoga na hujajiremba avutiwe na jinsi ulivyo na hicho kitakufanya ujiamnini na kujiona upo kwenye mikono salama.

Kuwa na mtu ambaye anakuthamini, anayeijua thamani yako, anayeyaweka mawazo yako mbele na akikosea hasiti kuomba msamaha, mtu ambaye ukiwa naye unajisikia Amani kuliko ukiwa na mwingine yeyote.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Translate

sam magelle

Main Menu Links

HABARI KALI ZAIDI

HABARI ZILIZOPITA

CHAGUA HABARI na sammagelle.com

Copyright © juu | Powered by Blogger