Ni vigumu sana kumuacha mtu umpendaye. Unapompenda mtu mara nyingi hufikirii kufanya maamuzi yoyote hasi. Akili yako kamwe haimuwazii mambo mabaya mwenzi wako.
Matamanio ya moyo wako ni kuona mnazidi kupendana. Mnazidi kuweka upendo mbele katika kila jambo linalowatokea katika maisha yenu. Upendo unawafanya muwe kitu kimoja katika maamuzi. Upendo unawapa faraja katika maisha yenu.
Upendo unawafanya mchukuliane kwa kila hali, mathalani masuala ya ugonjwa na matatizo mengine. Shida yako ni shida yake, ya kwake pia inakuwa yako. Upendo unapowazunguka wapendanao wanakuwa wanaishi katika ulimwengu wao.
Mkiishi katika misingi ya upendo, ni nadra sana kuona ugomvi kwa wapendanao. Pamoja na hayo, kuna wakati huwa yanatokea matatizo mbalimbali katika uhusiano ambayo kimsingi wakati mwingine yanapoteza ladha ya uhusiano.
Hii inaweza kujidhihirisha kipindi tu mnaanza uhusiano, wakati mwingine huwa inatokea mkiwa tayari kwenye kilele cha safari yenu. Mfano inaweza kutokea mkiwa katika hatua ya uchumba au inaweza kutokea mkiwa tayari kwenye ndoa.
Katika kushughulikia haya, kwa hatua hizi mbili muhimu kila moja ina namna yake ya kufanya maamuzi. Mnapokuwa katika uchumba, unashauriwa kuchuja uzito wa matukio husika na kama ukiona ni mazito na yanakukosesha furaha, ni bora kusitisha safari mapema.
Usikubali kuendelea na safari ambayo inaonesha ina changamoto nyingi kuliko suluhu. Maisha yana changa-moto nyingi hivyo ni vyema linapo-kuja suala la uhusiano liwe la faraja zaidi kuliko changamoto za maisha, uhusiano usigeuke kuwa kaa la moto.
0 comments:
Post a Comment