juu

Saturday, 7 September 2019

NJIA BORA, RAHISI YA KUISHI NA MPENZI ALIYE MBALI



MAPENZI ni hisia ambazo hazizuiliwi na mipaka ya nchi ama mabara katika kusafiri kwake.
Hisia zinapenya mbele ya uzio wa dini, kabila rangi na vipato, kawaida ya hisia za mapenzi ni kutengeneza daraja na si kujenga ukuta kwa watu.
Kama mtu ana hisia halisi za mapenzi juu ya fulani, hujikuta akimthamini, kumjali na kumtakia mengi ya heri bila kujali rangi yake, kipato chake na sifa nyinginezo.
Watu wengi kwa kutofahamu, huamini wapenzi wao wakisafiri na kukaa mbali kwa muda fulani basi inaweza kuwa chanzo cha wao kutopendwa na kuhitajika tena.
Katika dunia ya sasa yenye kila aina ya nyenzo za mawasiliano, kuwaza hivyo ni kosa kubwa, japo ni muhimu wapenzi kuonana ana kwa ana (physically).
Ila inapotokea kutoonana tena kwa sababu za msingi maana yake si imefika tamati ya uhusiano wenu.
Mapenzi ni hisia, ili mwenzako akujali na akuthamini, inabidi ucheze na akili yake hali itakayoshawishi hisia zake zikutazame wewe katika namna fulani bora.
Mwenzako akikuona wa thamani, bora na mwenye vingi vya kujivunia, ndiyo anaweza kuona wengi pengine na kuwasifia (kila binadamu ana tamaa, tunatofautiana katika namna ya kuziachia na kuzidhibiti), ila wewe daima kwake utabaki kuwa bora na mwenye thamani.
Kuna wengi wanaonana kila siku, wengine wanalala chumba kimoja ndani ya shuka moja ila hawana mshikamano wa kweli, kama wale ambao wanaoishi mbalimbali, kwa sababu wameshindwa kushikana kihisia vile inavyotakiwa.
Jiulize kwa makini, mwenzako anakutazama vipi? Anakuona ni binadamu tu au anakoshwa hasa na unavyomtendea, unavyomjali, unavyomfurahisha na kumpa raha na furaha?
Kama kupitia matendo na kauli yako unamfanya mwenzako akuone wa pekee, mtu ambaye una vingi vya kujivunia, basi anaweza kuona watu wengi ila kwako akajiona amebahatika sana kuwa na wewe.
Kinachotakiwa tu kwa kuwa mwenzako yuko mbali ni kudumisha mawasiliano yaani muongee ama mchati, ila pia katika kuchati huko ama kuongea, uhakikishe maongezi yenu mara nyingi yanawapa furaha, amani na msisimko.
Inabidi kwa gharama yoyote ujiepushe na migogoro isiyo na tija kupitia kuwasiliana kwenu, kwa watu walio mbalimbali migogoro ya kila siku inachefua kwa kasi hisia zao kwa kuwa yuko mbali na mwenzake.
Mmoja anaweza kujikuta anakabiliwa na wingi wa fikra hasi hali inayoweza kumfanya atafute sehemu ya kutua matatizo yake walau kwa muda.
Ukiwa unachati mara nyingi pendelea kuchati naye juu ya matamanio yake na vitu anavyopenda, zungumza naye mambo unayojua huwa yanampa raha na hamasa sana ama katika maisha au mahusiano.
Utabaki na udhibiti wa mwenzako hata akiwa mbali kama utafanikiwa kuamsha na kusisimua hisia zake kwa namna nzuri hata akiwa mbali.
Tatizo la wengi ni kwamba wakiwa mbali na wapenzi wao, hujikuta wakiacha kujiamini kabisa hali inayopelekea kila siku kuwatuhumu wenzao katika masuala mbalimbali ya usaliti, hatua inayoleta migogoro ya mara kwa mara katika uhusiano husika.
Hali hii inapoendelea husababisha hata msisimko wa wenzao kupungua kwao kitu kinachovunja muunganiko wa kihisia( breaking emotional connection), hivyo wenzao kuamua kuanzisha mahusiano mengine kwa sababu haya yaliokuwapo hayawapi tena sababu ya furaha wala matarajio mema.
Kuna aina ya migogoro inayochochea hali ya mapenzi kwa mwenzako ila ile ya kila siku hukera na kumfanya mtu ajutie kuwasiliana na wewe, kitu kinachofanya pia achukie kuwa na wewe katika maisha yake.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Translate

sam magelle

Main Menu Links

HABARI KALI ZAIDI

HABARI ZILIZOPITA

CHAGUA HABARI na sammagelle.com

Copyright © juu | Powered by Blogger