BILA shaka msomaji wangu uko poa, kwa wewe ambaye unasumbuliwa na shida mbalimbali za kidunia, nakuombea kwa Mungu upate ahueni. Wiki iliyopita tulianza kujadiliana kuhusu mada hii kama inavyojieleza. Je, wewe unaamini kwamba kwenye mapenzi kuna uchawi? Unaamini kwamba kuna kitu kinaitwa limbwata? Je, ni kweli mtu anaweza kwenda kwa mganga na akafanikiwa kumpumbaza mwenzi wake akili? Nakushukuru wewe uliyetumia muda wako kunipa majibu ya jinsi unavyoyaelewa mambo haya.
Majibu niliyoyapata yalikuwa katika makundi mawili; wapo waliosema wanaamini ni kweli kuna uchawi katika mapenzi, wakaenda mbali na kutoa mifano iliyowatokea au waliyoishuhudia na kuwafanya waamini kwamba kweli kuna uchawi katika mapenzi. Msomaji wangu mmoja kutoka Unguja, Zanzibar, alisema anao ushahidi wa jinsi mume wa rafiki yake alivyoendewa kwa mganga na kimada wake hadi akafikia hatua ya kutelekeza familia ya mke na watoto watatu, akahamia kwa kimada. Unaambiwa mpaka leo hasikii haambiwi, ameikana familia yake kisa kimada.
Kundi jingine lilisema haliamini katika uchawi! Kwamba mume kumsaidia mkewe kuosha vyombo, kufua, kupika, kumpa kila anachokitaka au kutii kila anachoambiwa, siyo lazima awe amerogwa bali akioneshwa mapenzi ya dhati, yupo tayari kufanya chochote ilimradi mwenzi wake afurahi! Kwa wale walionitumia ushuhuda kuhusu limbwata, wengine wakilalamika kwamba wenzi wao wamebadilishwa mawazo na wanawake au wanaume wa nje mpaka kufikia hatua ya kuwakana wapenzi wao wa awali kwa sababu ya ndumba, nataka waelewe kitu kimoja muhimu sana.
Mapenzi ya dhati yana nguvu kuliko hata mauti, vitabu mbalimbali vya dini vinathibitisha hili. Kwamba, ukimpenda na kumuonesha mapenzi ya dhati mwenzi wako, naye akakupenda, mkashibana, hakuna nguvu inayoweza kuingia katikati yenu, iwe uchawi, ndumba au majini na kuwatenganisha.
Hata kama kuna mtu anautazama uhusiano wenu kwa husuda, hata akikesha kwa waganga kwa lengo la kuwatenganisha ili yeye apate nafasi, ni sawa na kazi bure! Penzi la dhati lina nguvu asikwambie mtu! Hata hivyo, mapenzi ya dhati yanapokosekana ndani ya uhusiano, uwe ni uchumba, ndoa au mahusiano ya kawaida, ni dhahiri kwamba hata vitu vidogovidogo tu, vinaweza kuwatenganisha mkaishia kusingizia uchawi!
Kama hampendani, mtu anaweza kuingiza maneno ya kuwafitinisha tu, mkaachana. Kama hampendani kwa dhati, ugomvi mdogo tu, unaweza kuwatenganisha, kama ni ndoa ikavunjika, kama ni uchumba ukaishia njiani na mambo ya namna hiyo! Kwa hiyo jambo la msingi, siyo kukimbilia kwa waganga mambo yanapoharibika ukiamini mwenzi wako amerogwa na mpenzi wa nje. Unachotakiwa kufanya kuanzia sasa, kabla mambo hayajaharibika, ni kuhakikisha kila siku iendayo kwa Mungu, unaishi vizuri na mwenzi wako.
Mpende kwa dhati, kuwa mwaminifu, mjali, msamehe anapokosea, mtimizie mahitaji yake ya msingi na usichoke kumrekebisha kwa njia nzuri ili mwisho aje kuwa bora!
Mkiishi hivi, hata atokee mchawi kutoka kuzimu, wala hawezi kuvunja ndoa yenu wala wewe hutahitaji kwenda kwa mganga ili kumroga au kumpumbaza akili asikuache, mapenzi yako ndiyo yatakayokuwa uchawi tosha. Lakini ikitokea mkaishi kwa mazoea tu, hakuna mapenzi ya dhati ndani ya nyumba, kila mmoja anajiona yeye ni bora, kiburi, dharau, usaliti, maudhi, uongo na kero za namna hiyo zimetawala, uhusiano wenu hauwezi kwenda popote na ninyi ndiyo mtakuwa wachawi wa penzi lenu.
Hata ukihangaika kwa mitishamba na hirizi, kama humuoneshi mapenzi ya dhati mwenzi wako, ni kazi bure! Siku akimpata anayemjali na kumuonesha mapenzi ya dhati, itakula kwako. Ni hayo tu kwa leo, tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine murua.
0 comments:
Post a Comment