Siku chache zilizopita, nilitembelewa na mmoja wa wasomaji wangu aliyekuwa akihitaji msaada wa kimawazo kutokana na majanga yaliyokuwa yakimkabili. Alichoniambia ni kwamba, amefarakana na mchumba’ke mtarajiwa kiasi cha mwanaume huyo kufikia hatua ya kutishia kuvunja uchumba.
Chanzo cha matatizo yao, ni baada ya mwanaume huyo kumtembelea ghafla mwanamke huyo nyumbani kwake bila kumpa taarifa, lakini katika hali ya kushangaza, alimkuta akitoka kwenye chumba cha mpangaji mwenzake wa kiume.
“Huwa nina kawaida ya kwenda kwa huyo mpangaji mwenzangu na yeye huwa anakuja kwangu, tumezoeana kama kaka na dada na huwa tunasaidiana mambo mengi, hakuna chochote kinachoendelea kati yetu, tumezoeana tu,” alisema dada huyo huku akilia.
Anasema mchumba’ke anamtuhumu kwamba anatoka naye kimapenzi ndiyo maana wamezoeana kiasi hicho! Jamaa amekasirika sana na hataki tena kusikia chochote kutoka kwake, uchumba wao upo mashakani.
Ni sababu hiyo ndiyo iliyonisukuma kuja na mada hii leo. Unaweza kuona jinsi mazoea yasiyoyofaa yanavyoweza kusababisha matatizo makubwa katika uhusiano wa kimapenzi. Wanandoa wengi wanatengana na kupeana kabisa talaka kwa sababu tu ya mazoea yasiyofaa, mapenzi yanavurugika, uchumba unavunjika.
Jambo ambalo kila mtu anapaswa kulijua ni kwamba huwa hakuna urafiki wa kawaida kati ya mwanaume na mwanamke. Huwezi kuwa na mazoea na mwanaume fulani wakati unaye mpenzi wako, halafu ukasingizia kwamba ni rafiki tu! Huwezi kuwa na mazoea na msichana au mwanamke mwingine halafu ukasingizia kwamba ni rafiki tu.
Kwa taarifa yako, mazoea ya mwanamke na mwanaume ambao hawana uhusiano wa kimapenzi, huishia kwa wawili hao kuwa wapenzi. Utafiti wa kisayansi unaonesha kwamba kadiri mnavyozidi kuzoeana, ndivyo mnavyozidi kuwa karibu kihisia. Ukaribu wa hisia, huzaa hisia za kimapenzi na mwisho mtajikuta mkiangukia dhambini, wakati mwingine bila hata kuelezena hisia zilizo ndani ya mioyo yenu.
Unapokuwa kwenye uhusiano, suala la kutofautiana au kugombana huwa ni kawaida. Unapokasirika, unapenda kumshirikisha rafiki yako kwa ajili ya ushauri na hapa ndipo makosa makubwa yanapoanzia.
Ukifuatilia kwa undani, utagundua kwamba mwanamke na mwanaume wanapokuwa na mazoea ya kupitiliza, huelezana mambo yanayohusu uhusiano wao wa kimapenzi.
Kama mkeo amekukwaza, utamweleza rafiki yako huyo wa kike, kama mumeo amekuudhi, utamweleza rafiki yako huyo uliyezoeana naye, atakupa ushauri kulingana na kilichotokea.
Atakufariji, atajitahidi kukufanya uwe sawa, ataonesha kukujali. Hali hii ikiendelea, taratibu utaanza kumuona yeye kuwa ni bora kuliko mtu wako! Utaanza kuona anakujali kuliko mpenzi au mume aumke wako na hapa ndipo hisia za mapenzi zinapoanzia.
Nini cha kufanya? Hukatazwi kuwa na marafiki wa jinsia nyingine, lakini unapaswa kuwa na mipaka. Ukishindwa kuweka mipaka, maana yake ni kwamba unatengeneza tatizo ambalo baadaye litakuja kukugharimu.
Kinachomliza dada huyu leo, ni tatizo ambalo mwenyewe alilikaribisha, anavuna alichopanda. Ni sawa kwa mwanaume kukasirika kwa sababu hakuna mtu anayependa kuona mtu anayempenda na kumjali, anakuwa na mazoea ya kupitiliza na mtu wa jinsia tofauti kwa sababu anajua mwisho wake utakuwa ni nini.
0 comments:
Post a Comment