juu

Monday, 3 June 2019

MATUMIZI HOLELA YA DAWA YANAVYOSABABISHA SARATANI

KITENDO cha mwanamke kutumia kiholela dawa za uzazi wa mpango humuweka katika hatari kiafya hasa kupata kansa ya kizazi.  Kibaiolojia wanawake wana uwezekano mkubwa kupata saratani kwa kiwango cha asilimia 100 kuliko wanaume. Tatizo hilo linahusishwa zaidi na homoni ya Oestrojeni ambayo kiasili wanawake ndio ambao wanazo zaidi kuliko wanaume.

Dawa za uzazi wa mpango zinatakiwa kutumiwa vizuri kwa ushauri wa daktari kwani kuna wengine zinawasumbua. Kuna mabinti na wanawake wanakwenda tu kujinunulia wenyewe kwenye maduka ya dawa, hiyo ni hatari kwao. Dawa zozote ni lazima upatiwe na daktari kwa sababu yeye anao uwezo wa kukuangalia na kukutathmini.

Mara nyingi dalili za kansa huanza kujitokeza mtu anapokuwa na umri kati ya miaka 15 hadi 20 lakini kwa kuwa wengi hawana mwamko wa kupima afya zao mara kwa mara hugundulika kuwa na ugonjwa hasa wakiwa na umri wa kuanzia miaka 40. Kwa asilimia tano tu mtu huweza kupata ugonjwa huo kwa kurithi kutoka kizazi kimoja hadi kingine.

Kitendo cha mama anayetakiwa anyonyeshe kutonyonyesha mtoto kunaongeza hatari ya kupata ugonjwa wa saratani ya matiti. Matiti kwa mwanamke yana kazi kuu mbili, kwanza ni kutengeneza chakula kwa ajili ya mtoto wake lakini pili ni kutengeneza umbo lake (urembo).

Tatizo tunaloliona leo hii la saratani ni kwa sababu wanawake wengi hawapendi kunyonyesha watoto wao kwa hofu ya kupoteza ule mwonekano wao, bila kujua kwamba kufanya hivyo kunasababisha kuharibu mpangilio wa mwili na hivyo kuwa kwenye hatari ya kupata saratani.

Kuna visababishi vingine ambavyo kwa kiwango kikubwa vinachangiwa na mfumo mbovu wa maisha yetu ya kila siku. Vyakula vya kusindikwa vyenye kemikali vilivyo kwenye makopo au chupa na mafuta mengi vinavyosababisha ongezeko kubwa la uzito wa mwili na vinywaji vyenye sukari nyingi inaweza kuwa sababu ya kupata saratani. Sababu nyingine ni uvutaji wa sigara na matumizi ya bidhaa zilizotengenezwa kwa kutumia tumbaku, unywaji wa pombe na matumizi ya maji yaliyochafuliwa kwa kemikali (water pollution) ni chanzo cha saratani.

Vitu hivyo huharibu mpangilio wa seli na kuuvuruga. Kibaiolojia mwili wa binadamu umejengwa kwa chembechembe hai ziitwazo seli ambazo ndizo hutengeneza viungo mbalimbali na mfumo mzima wa mwili wa binadamu. Chembechembe hizo huwa na tabia ya kugawanyika, kukua na kupevuka ili ziweze kutengeneza mwili na kwamba huwa kuna mpangilio maalumu wa jinsi zinavyokua, kugawanyika na kupevuka kulingana na wakati.

Sasa inapotokea utaratibu huo wa kawaida ukavurugika basi hapo seli hizo hukua, hugawanyika na kupevuka bila mpangilio maalumu na hivyo kusababisha saratani. Saratani ni ugonjwa ambao upo katika kundi linalojumuisha magonjwa yasiyokuwa ya kuambukiza ambao husababisha vifo vya idadi kubwa ya watu. Kwa upande wa hii saratani ya matiti takwimu za dunia zinaonesha inashika nafasi ya pili duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa.

Kasi ya ugonjwa inaonekana kuwa juu zaidi na inakadiriwa ifikapo mwaka 2030 ikiwa hatua hazitachukuliwa kukabiliana na ugonjwa huo, idadi itaongezeka mara dufu kufikia asilimia 50 katika nchi zinazoendelea.

Saratani hiyo inashika nafasi ya pili kwa kundi la wanawake kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa na inashika nafasi ya nne kati ya saratani zote zinazogundulika nchini. Hali hiyo inachangiwa na uelewa mdogo wa jamii juu ya ugonjwa huo pamoja na imani potofu kwa wengi kukimbilia kwa waganga wa kienyeji wakidai wamerogwa.

Hata wale wanaofika hospitalini huwa wapo katika hatua mbaya hivyo matibabu yake huwa ni magumu. Wale wanaowahi katika hatua ya kwanza na ya pili ya ugonjwa wakipatiwa matibabu hupona kabisa lakini si hatua ya tatu na nne.

DALILI ZA UGONJWA

Kwa kuwa yale ni mabadiliko ya chembechembe hai mara nyingi huwa yanatokea ndani ya mwili ambako hatuwezi kuona dalili kwa nje katika hatua ambayo zimeanza kukua au kugawanyika, tunachoweza kuona kwa nje ni uvimbe, ongezeko la titi, uzito wa titi na maumivu makali.

Uvimbe unapokuwa mkubwa wakati mwingine husababisha kukandamizwa kwa mishipa ya damu na inapopasuka chuchu huanza kutoa damu.

Uvimbe huweza pia kubadili mwonekano wa chuchu na kuzifanya ziwe kama ganda la limao wakati mwingine huvuta chuchu kwa ndani na au kuzifanya kuwa ngumu. Pia zinaweza kutoa kidonda na uvimbe ukiwa mkubwa zaidi husambaa kuelekea sehemu za kwapani, ukichelewa kupata matibabu saratani husambaa hadi kwenye viungo vingine vya mwili ikiwamo mifupa, mapafu na hata moyo.

MATIBABU

Ili kuuondoa uvimbe mgonjwa hufanyiwa upasuaji. Matibabu ya pili huwa ni kuwapatia tiba ya mionzi ili kuzuia seli ambazo hazikuonekana awali.

Saratani huwa inasambaa kwa njia ya damu na kwa kuwa zina tabia hii, huwa wagonjwa wanapatiwa dawa ya saratani za dripu (Chemotherapy), wale wenye vichocheo vingi vya homoni huwa tunapewa Hormonaltherapy pia dawa za kutuliza maumivu na nyinginezo kulingana na hali ya mgonjwa husika.

USHAURI

Ni muhimu kuzingatia ulaji unaofaa hasa vyakula vyenye virutubishi vinavyohitajika mwilini, mazoezi mara kwa mara, kunywa maji ya kutosha na kupima afya mara kwa mara.

 Na mtaalam wetu, A.Mandai

The post MATUMIZI HOLELA YA DAWA YANAVYOSABABISHA SARATANI appeared first on Global Publishers.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Translate

sam magelle

Main Menu Links

HABARI KALI ZAIDI

HABARI ZILIZOPITA

CHAGUA HABARI na sammagelle.com

Copyright © juu | Powered by Blogger