juu

Monday, 3 June 2019

UKIMPATA MTU SAHIHI, MSHIKILIE KWELI KWELI

Moja kati ya kosa kubwa ambalo watu wengi wanalifanya ni kutothamini hisia. mahusiano mengi yamevunjika kwa sababu tu ya mmoja kati ya wapendanao kutotambua umuhimu wa penzi lao na mwisho wa siku wanajikuta wameachana. Mimi na wewe msomaji wangu ni mashahidi wa hili. Kwenye dunia ya wapendanao sasa hivi, wengi sana wamejikuta kwenye majuto baada ya kushindwa kushikamana kwenye mikono salama.

Mwanamke anaweza kuwa kwenye uhusiano na mtu sahihi, anakikuta amemuachia. Vivyo hivyo mwanaume, anaweza kuwa na mtu sahihi katika uhusiano wake lakini anajikuta ameipoteza bahati ya kuwa na mpenzi wake huyo hadi mwisho wa safari sababu tu ya kushindwa kuheshimu umuhimu wa safari yao. Hii inatokana na mtu kuleta mazoea kwenye penzi. Wakati mwingine inasababishwa na dharau ya mtu. Anapomuona mwenzake anamheshimu, anampenda na anamthamini, kwake inageuka kama fimbo ya kumchapia.

Analeta maringo, anaanza kuleta pozi na inapotokea mwenzake amekata tamaa na kuanzisha uhusiano mwingine, anajikuta akijilaumu. Kwamba alikuwa na mtu sahihi lakini hakumthamini na matokeo yake anataka kurudisha majeshi lakini anakuwa ameshachelewa. Ndugu zangu, thamani ya mtu mara nyingi huwa inaonekana pale anapokuwa hayupo.  Anapokuwepo unaweza kuwa unamchukulia poa lakini akiondoka unaanza kumkumbuka na kutambua ule uwepo wake na kuona kwamba haukupaswa kuupoteza. Kwa nini usubiri majuto? Kwa nini usiitumie vizuri leo yako ili uweze kuishi vizuri na mtu ambaye ndio chaguo lako.

Mtu ambaye kweli unampenda kutoka moyoni. Mtu ambaye moyo wako ukiwa naye unapata furaha, unaachaje kumjali? Kwa nini usimtunze kama mboni ya jicho lako? Kabla ya kumfanyia vituko, kabla ya kuanza kumuonesha kejeli, dharau na mambo mengine kama hayo, hakikisha unajiuliza mara mbilimbili kwamba ninayemfanyia hayo yote anastahili? Jiulize je,  uliye naye ni mtu sahihi kwako? Unampenda kwa dhati? Na yeye anakupenda kama unavyompenda wewe? Anakujali? Hana kipingamizi chochote cha kuwa na wewe? Mnaelewana? Ukipata majibu chanya kuhusu maswali hayo, shikamana na huyo mtu. Ninasema shikamana naye sababu naye anastahili

kushikamana na wewe. Mpende, mthamini na umuone ni mtu wa muhimu katika dunia hii kuliko kitu chochote. Mueleze naye aujue umuhimu huo maana jahazi lenu litakapoangamia, mtaishia kujilaumu. Mnayo nafasi kabla ya kulaumiana, msiruhusu kisingizio cha shetani. Mkataeni huyo shetani sababu Mungu amewapa akili na upeo wa kutambua mema na mabaya. Heshimu hisia za mwenzako ili naye akuheshimu. Kila iitwayo leo, fanya jambo kwa ajili ya kuonesha upendo kwa mwenzako.

Aone unamjali na unamthamini. Hata kama si jambo kubwa, fanya hata dogo. Mathalani unaweza hata kumjulia hali baada ya kupita ukimya wa muda fulani. Mpigie simu muulize anaendeleaje, ameshindaje na mambo mengine madogomadogo ambayo yanaweza kumfanya mwenzako ahisi unamjali. Guswa na matatizo yake.

Kama anaumwa, mjulie hali ya kuumwa kwake ikiwezekana hata baada ya saa fulani kupita. Mpe zawadi ndogondogo au hata kubwa kulingana na uwezo wako. Mfanye mwenzi wako kila siku akufurahie maana furaha yake ni wewe. Akiikosa kwako ataipata wapi kwingine? Mpende kwelikweli kama hutapenda tena.  Usimtegee, mrudishie upendo kama anavyokupenda wewe. Tambua uwepo wake hata unapokuwa mbali naye. Heshimu dhamira na mipango yenu mliyojiwekea. Usikubali hata kidogo kumpoteza mtu ambaye mna mipango ya kufika mbali katika uhusiano wenu.

Kwa leo naishia hapa. Tukutane wiki ijayo. unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii, instagram na facebook natumia jina la erick

The post UKIMPATA MTU SAHIHI, MSHIKILIE KWELI KWELI appeared first on Global Publishers.


Share:

0 comments:

Post a Comment

Translate

sam magelle

Main Menu Links

HABARI KALI ZAIDI

HABARI ZILIZOPITA

CHAGUA HABARI na sammagelle.com

Copyright © juu | Powered by Blogger