juu

Thursday, 7 November 2019

HAKUNA ASIYEPENDA KUPENDWA



Katika jamii yetu kutongoza halionekani kama ni jambo jema sana, hata kama dhamira yako katika kufanya hivyo ni ndoa. Linaonekana kama ni jambo la utovu wa maadili.

Hilo linawafanya watu wengi wahofie kuwataka kimapenzi watu wanaowapenda, hasa wale wanaowaheshimu.

Ndio maana utakuta vijana katika makundi mbalimbali ya kijamii, watapata shida kuwekana bayana juu ya mapenzi kwa kuhofia kuwa wataonekana hawana maadili, au utaonekana humuheshimu.

Unaweza kumfuata msichana au mvulana ukamtaka kuanzisha uhusiano wa kimapenzi akakujibu,

‘Yaani nilikuwa nakuheshimu sana kumbe wewe ni hovyo kabisa’ au akakujibu, “mimi nakuheshimu sana, sasa tunawezaje kuwa wapenzi”.

Yaani inaonekana kama vile mapenzi ni kwa wale wasioheshimiana. Kwa maoni yangu huu sio mtazamo sahihi. Ukimkabili msichana au mvulana, jambo analoweza kukuuliza ni, “Una nia ya dhati au unataka kunichezea”.

Lakini dhana hii potofu katika kutongoza sio kwamba imekuwepo kutokana na hulka mbaya ya jamii yetu, la hasha. Ni kwa sababu safari zetu nyingi za mapenzi katika jamii yetu huwa hazifiki katika ndoa, huwa zinaishia njia panda.

Ukianza kumuuliza kijana yoyote tangu akue, ameshakuwa na mahusiano na watu wangapi, na kama kila mtu akiamua kutaja kwa uaminifu unaweza kustaabu majibu yake.

Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kuwa anaweza kujaza fuso zilizopangana kutoka Posta mpaka Ubungo kwa wanaoijua Dar es Salaam. Au niseme si chini ya Kilometa 10.

Hata pia ukiwauliza wanandoa, kabla ya kuoana wameshawahi kuwa na wapenzi wangapi, majibu hayatatofautiana sana na kundi la vijana ambao hawajaoana, japo wapo wachache ambao wamefanikiwa kuwa na idadi ndogo sana ya wapenzi kabla hawajaoana.

Ni dhahiri kuwa tunatakiwa kuwa makini tunapofanya uamuzi wa kuanzisha maisha ya kimapenzi kwa kulenga katika ndoa zaidi kwa kuwa hatuwezi kujinasua kutoka katika maisha ya kimapenzi tunapokuwa hapa duniani.



Hofu ya kupigwa kibuti Pengine hili ndilo linalowakumba walio wengi.

Akinadada ndio waathirika zaidi ya hili kuliko wanaume kwa sababu inaonekana kama ni jambo la aibu sana kwa msichana kukataliwa na mvulana. Anaweza akampenda mvulana, lakini akaishia kuonyesha dalili tu, au kwa lugha ya wavuvi unaweza kusema kuita ‘akaamua kulishia’ tu.

Na kama mwanaume hatachukua hatua, basi msichana huyo atataabika mpaka anafanya vitendo vya aibu. Katika jamii yetu, msichana au mvulana akikukataa ni jambo la aibu.

Kama uko chuoni, kazini au sehemu yoyote yenye mjumuiko, hutatamani suala hilo walijue watu wengine zaidi ya mhusika.

Eti ni aibu! Rafiki yangu mmoja aliwahi kuniambia kuwa ukiona unashindwa kujiweka wazi kwa mtu unayempenda, basi bado hujakua kiumri. Hizo ni dalili za utoto na unaweza kuwa mtu mzima kiumri, lakini ukawa ni mtoto kimapenzi.

Wapo watu wazima ambao hawajapata wenza wa kimaisha, wengine ni mabosi maofisini, wanaopata kigugumizi kueleza hisia zao kwa wanaowapenda.

Yaani wanaonesha dalili tu au anaweza kukualika hadi nyumbani kwake, akifika huko na akashindwa kukueleza zaidi ya kuonesha kila dalili kuwa anakupenda. Hata hivyo unaweza kukabiliana na changamoto hizo kwa kufanya yafuatayo.

Jiamini kama unaweza. Wanasema uzuri wa mtu uko kwenye macho yake. Ni kama utamu wa pipi unavyotegemea mate ya mmung’unyaji.

Unatakiwa kujiamini kuwa unaweza kufanikiwa kuwa na mahusiano na mtu unayefikiria kumfuata. Unaweza kukuta kuwa na yeye anakufikiria wewe ila hajakutamkia tu.

Lakini hata kama bado hajakufikiria, unaweza kubadili mawazo au msimamo wake kwa sababu wapo watu waliowashawishi wapenzi wao ambao awali wali- kuwa wanawachukia sana.

Ndio maana unaweza kukuta wapenzi wanakumbushana, “Lakini zamani nilikuwa nakuchukia wewe, sijui ilikuwaje ukaninasa”.



Hakuna mtu asiyependa kupendwa. Anaweza kujisikia furaha sana akijua kuwa kuna mtu anampenda. Jambo la msingi ni kuwa mueleze na muoneshe kuwa unampenda mpaka akuamini na jitahidi asije akakuona ‘msanii’.

Mwanzo ndio kila kitu. Katika suala hili, ukikosea mwanzo, unaweza kuwa na mwisho mbaya.

Na hakuna fomula ya jinsi ya kuanza, inategemea mko katika mazingira gani, unaongea na nani na mnafahamiana vipi.

Kama mnafahamiana, inaweza kuwa rahisi zaidi, lakini kama ndo mara ya kwanza kufahamiana, unaweza kuanzisha mazoea kwanza kabla ya kwenda kwenye pointi kwa sababu binadamu huwa ana kawaida kutomuamini mtu asiyemfahamu.

Na katika hili la kuzoea, sio lazima iwe baada ya wiki moja, mwezi au mwaka, mtu anaweza kukuzoea kwa nusu saa tu na akakuamini kwa kila unachomuambia. Ni vizuri kuzoeana kwanza kabla hujarusha ndoano.

Wakati uko katika kuzoea, lazima uwe unajua lengo lako ni nini, wazungu wanasema unatakiwa kuwa objective. Kila unapokuwa unaendelea kumzoea tambua kuwa unatafuta wakati muafaka wa kuingiza hoja yako.

Na wakati ukifika, ingiza hoja yako mara moja kwa sababu ukichelewa ni tatizo, lakini pia ukiwahi kabla ya wakati ni tatizo kubwa zaidi.

Wakati mwingine unaweza kuahirisha kuingiza hoja yako ukatafuta siku nyingine. Na unapoahirisha, hakikisha kuwa kweli wakati wa kuingiza hoja ulikuwa haujafika kwa sababu kama wakati ulishafika, matarajio ya mtarajiwa wako ni kuwa ‘utawasilisha’ na usipowasilisha anakuona kama muoga na usiyejiamini.

Ni rahisi kumpoteza. Jambo la msingi ni kuwa unatakiwa kumvutia mtarajiwa wako kiasi kwamba hata ukiingiza hoja yako akujibu, “Nilikuwa naisubiria sana fursa ya kuwa nawe, nashukuru nimeipata”.

Jinsi ya kumvutia ni kama ifuatavyo:- Wakati unamzoea kwa maongezi ni vizuri ukatafuta ni kitu au jambo gani analolipenda na ukishalitambua litekeleze kwa ufanisi.

Akishabaini kuwa wewe ni nguli katika jambo analolipenda, atakupenda nawe pia. Kuna nguvu kubwa sana ya kimapenzi iko machoni.

Kwanza ukimtazama utamuonesha kuwa unajiamini na unapojiamini ni dalili kuwa unafanya jambo lisilo la hila. Waswahili husema mkamia maji huwa hayanywi. Ni sawa na kanuni ya uhitaji, kwamba vitu unavyovihitaji sana ndivyo ambavyo huadimika zaidi.

Hata yeye ukimhitaji sana ataadimika. Kama umeshafanya sehemu ya kwanza vizuri ya kujizoesha kwake na kutekeleza kwa makini kile anachokipenda, lazima kuna kipindi atakuwa anakutafuta.

Akikutafuta hiyo ni dalili tosha kuwa anaku-“miss” na hapo ndipo utakuwa unaelekea kuweka mpira ndani ya kimia. Hakuna binadamu anayependa kuwa na mwenza asiyethaminika katika jamii. Na katika suala hili la kuchagua wenza, wengi huwa wanaangalia, “Nikiwa naye jamii itanichukuliaje”.

Jamii ikikukubali, ni rahisi sana na yeye kukukubali. Ndio maana nyota katika michezo huwa hawana kazi ngumu ya kupata wenza wao.

Wanaowapenda ‘hujigonga’ hata kabla hawajawatongoza. Sio kwa sababu unampenda kila anachokuambia unafanya. Kataa kufanya ujinga na usidhani kuwa ukikataa ndio umemkosa, bali utakuwa umemuonesha jinsi ulivyo makini.

Na hata atakavyobaini kuwa jambo ulilokataa kulifanya lilistahili, atajiona yuko na mtu ambaye atasahihisha makosa yake pale atakapokuwa anakosea.

Jambo la maana ni kuwa mfanye aelewe hoja yako kwa nini umekataa kutekeleza na unapofanya hivyo, tumia lugha nzuri isiyokarahisha.

Hakuna njia moja ya kuweza kufikisha hoja kwa unayempenda. Zipo njia nyingi, jambo la kuzingatia ni muda gani wa kufikisha hoja, mazingira gani yanayostahili, unayezungumza naye yuko katika hali gani.
Share:

0 comments:

Post a Comment

Translate

sam magelle

Main Menu Links

HABARI KALI ZAIDI

HABARI ZILIZOPITA

CHAGUA HABARI na sammagelle.com

Copyright © juu | Powered by Blogger